MASHAIRI YETU  
l
 Mashairi
Yetu
Lala kwa Kadri
Asiliye Wapi?
Vijulanga Bandilikeni
Ulimi wanikanganya

 

 

Chumba cha Majadiliano>>>  Tuma Maswali/majibu>>>
 
Ulimi Wanikanganya Na Martin Munywoki
Na Martin Mutua Munywoki
Nashindwa ewe ulimi, uko hapa ama pale?
Yakini hata uvumi, kilele cha makelele,
Nambie kama ni mimi, nilebuni jambo lile,
Ulimi wanikanganya, haki mbona sikwelewi,

Kidogo kiungo hiki, kimbelembele kinacho,
Umezua nyingi dhiki, kwa chote wingiliacho,
Iwapo haupayuki, tanipa nitafutacho,
Ulimi wanikanganya, haki mbona sikwelewi,

Hiki nisile wanambia, lakini kile nikile,
Tena kwa kunikazia, punde kakitema kule,
La kunena kiamua, msemi wasema lile
Ulimi wanikanganya, haki mbona sikwelewi,

Kila nifichapo siri, ulimi ukaitoa,
Kifumba yenye dosari, haikosi kayatoboa,
Kiwaza pate la kheri, hali mbichi kaling’oa,
Ulimi wanikanganya, haki mbona sikwelewi,

Kila nipate wateja, mbio ukawatimua,
Nipatanapo na waja, mbona unaingilia?
Marafiki kuwataja, mbali wawafukuzia,
Ulimi wanikanganya, haki mbona sikwelewi,

Wanibariki kwa wema, sitoshe kanilaani,
Wanibusu wanitema, wanuia haswa nini?
Watupa au watuma, wasimama ‘pande gani,
Ulimi wanikanganya, haki mbona sikwelewi,

Kitambo kutamatisha, tuzitunze ndimi zetu,
Tusije kajipotosha, ovu tukatae katu,
Ulimi taturidhisha, kiyaacha mambo butu,
Ulimi wanikanganya, haki mbona sikwelewi,
 

 


Haki zote zimehifadhiwa. Kunakili Makala yoyote kutoka Kwenye Tovuti Hii Bila Idhini Iliyoandikwa na Wakurugenzi Hakuruhusiwi. Makala yote yanamilikiwa na Gskool.com punde tu yanapotumwa.
Tuma Mchango wako
au maswali kwa kiswahili@gskool.com.
Home 
Forums and Discussions  Legal  Contacts  Faqs

©Gskool Educational Site