MASHAIRI YETU  
l
 Mashairi
Yetu
Lala kwa Kadri
Asiliye Wapi?
Vijulanga Bandilikeni
Ulimi wanikanganya

 

 

Chumba cha Majadiliano>>>  Tuma Maswali/majibu>>>
 
Lala kwa Kadri  Na Chrispus Munywoki
Lala ewe mlalaji, endelea ukitaka,
Lala unavyohitaji, moyo wako kuridhika,
Lala ingawaji, lakini hutatosheka,
Lala lakini kumbuka, masaibu wajitwika.

Lala juu kitandani, utakavyo burudika,
Lala hata godoroni, jifunike nazo shuka,
Lala ukijiamini, lakini kesho kumbuka,
Lala lakini kumbuka, masaibu wajitwika.

Lala tu baba mzazi, taabu waialika,
Lala we mama mzazi, wanao wataabika,
Lala takosa mchuzi, ufukara takushika,
Lala lakini kumbuka, masaibu wajitwika.

Lala tu mfanyakazi, mwajiri takasirika,
Lala taikosa kazi, na kubaki kiteseka,
Lala ewe mpukuzi, kisha utafedheheka,
Lala lakini kumbuka, masaibu wajitwika.

Lala shuleni shababu, uwe wasoma majaka,
Lala lalia vitabu, mwisho utatatarika,
Lala takosa jibu, mtihani ukifika,
Lala lakini kumbuka, masaibu wajitwika.

Lala tangu hizo zama, si rahisi kutoroka,
Lala milele daima, kwa miaka na mikaka,
Lala tu bila azima, lakini utasusurika,
Lala lakini kumbuka, masaibu wajitwika.

Lala ukiwa tajiri, mwisho utaporomoka,
Lala na wewe fakiri, utakosa unachotaka,
Lala bila kufikiri, utajuta bila shaka,
Lala lakini kumbuka, masaibu wajitwika.

Lala ewe mwanadamu, lakini yaja shabuka,
Lala itakulazimu, mwishowe kulalaika,
Lala utajilaumu, ninakusihi amka,
Lala lakini kumbuka, masaibu wajitwika.
 

 


Haki zote zimehifadhiwa. Kunakili Makala yoyote kutoka Kwenye Tovuti Hii Bila Idhini Iliyoandikwa na Wakurugenzi Hakuruhusiwi. Makala yote yanamilikiwa na Gskool.com punde tu yanapotumwa.
Tuma Mchango wako
au maswali kwa kiswahili@gskool.com.
Home 
Forums and Discussions  Legal  Contacts  Faqs

©Gskool Educational Site