MAMBO MUHIMU YA KUZINGATIA KATIKA UCHAMBUZI WA SHAIRI

1. Muundo

Eleza jinsi shairi lilivyoundwa, mpangilio wake,umbo lake. Angalia:

 • Beti: Idadi ngapi ya beti? Kila ubeti una mishororo mingapi?
 • Vina: Vina vya nje na vya ndani vichunguzwe. Kuna urari wa vina au la?
 • Kituo: Mshororo wa mwisho umerudiwarudiwa? ( shairi lina kibwagizo au la?) Mshororo wa mwisho umefupishwa?( bahari ya msuko)
 • Mishororo: Kila mshororo una vigao vingapi? Idadi ya mizani katika kila kigao? Maneno yamepangwaje?( chunguza mpangilio wowote maalum unaoibua dhana ya bahari fulani kama vile pindu, kikai, kikwamba, nk
 • Mizani: Idadi ya mizani katika kila mshororo?

2. Utoshelezi

Sharti shairi liwe na wazo linaloendelezwa. Chunguza kama  maudhui yameendelezwa na kukamilishwa kimantiki.

3. Muktadha

Mukatdha wa aina gain? Ni sifa zipi zinazojitokeza kisiasa, kiuchumi, kijamii, kikazi, nk? Muktadha hutuelekeza kwenye maudhui na dhamira.

4. Falsafa ya mwandishi

Huu ni msimamo wa malenga kuhusu suala linalorejelewa katika shairi. Maoni yake kuhusu jambo fulani ni yapi?

5. Mbinu za lugha:

Tamathali gani za usemi zilizotumika? Malenga ametumiaje fani mbalimbali kutosheleza maudhui yake? Km, methali, takriri, istiari…

Kumbuka kwamba:

 • Ukwapi ni kipande cha kwanza cha mshororo
 • Utao ni kipande cha pili cha mshororo
 • Mwandamizi ni kipande cha tatu cha mshororo
 • Mwanzo ni mshororo wa kwanza katika ubeti
 • Mloto ni mshororo wa pili katika ubeti
 • Mleo ni mshororo wa tatu katika ubeti
 • Kituo/ Kimalizio ni mshororo wa mwisho katika ubeti
 • Kibwagizo/ Mkarara ni kituo kilichorudiwarudiwa katika kila ubeti
You can leave a response, or trackback from your own site.

Andika Maoni/Jibu