|
'Kizazi kilichosoma hutarajiwa
kukuza na kuleta maendeleo kwa jamii husika.' Kwa kuirejelea riwaya ya
Mwisho wa Kosa na Z. Burhani, eleza maudhui ya elimu kama
yanavyosawiriwa katika riwaya hii. (alama 20)
Elimu ni mafunzo, masomo au
ujzi unaompa mtu
maarifa na hekima ya kuweza kulitekeleza jambo fulani
linalohitaji ujuzi huo.Kulingana na kazi ya mwandishi wa riwaya hii ya
Mwisho wa Kosa, kuna aina mbalimbali za elimu kama vile elimu ya dini,
elimu ya vitabu, elimu ya mabuku, elimu ya kuzaliwa na pia elimu ya
kujifunza kutoka kwa jamii ya mtu anamotoka.
Hata hivyo, mtu
anaweza kuwa mjinga ingawa amefanya juhudi sana ili kujipatia elimu ya
vitabu. Mathalan, mhusika Hasani, mumewe Muna, alikuwa amepata elimu ya
mabuku iliyomwelesha kupata kazi lakini hakuwa ameipata elimu ya dunia
ambayo ingalimwezesha kuishi vyema na mkewe. Aidha, Hasani hakutaka
kufanya uchunguzi zaidi kuhusu kazi yake na kwa hivyo hakutaka
kukiendeleza kiwango cha elimu yake.
Kulingana na jamii
hii, elimu ilikuwa imenuiwa kuweza kumtoa mja katika hali duni ya
umaskini na ufakiri na pia ujinga uliowafunga wengi wasijue jinsi ya
kutekeleza majukumu yao katika jamii. Pia, ilinuiwa kuweka msingi bora
wa maisha na kwa hivyo, ili kupata kazi nzuri, mtu hakuwa na budi kuwa
na elimu bora na ni katika kauli hii ambapo Ali alipofukuzwa shuleni
alilazimika kuifanya kazi ya hali ya chini madhali hakuwa na uwezo
kumwezesha kujichagulia kazi.
Wananchi katika
jamii hii waliitilia maanani na umuhimu elimu kwa vijana ni kwa sababu
hii kupitia kwa msaada wa serikali Monika na Muna walipata fursa ya
kusoma nao wanajamii wa jamii ya Monika walijawa na furaha riboribo
walipopokea habari za kufuzu kwa Monika. Walitarajia kuwa Monika
angewasaidia katika kukidhia mahitaji hasa katika familia yake
Monika.Hivyo, kuna vijana waliopelekwa ughaibuni au ng'ambo ili
kunufaika na masomo ya juu k.m. Monika, Muna na Hasani.Wengi walisomea
katika vyuo vikuu vya nchi yao vilivyokuwa vimeanzishwa na serikali k.v.
Ali na Ramadhan.
Hata hivyo, kuna
watu wasiojua kusoma wala kuandika, haswa wale waliokuwa wazee kama vile
Bi. Tatu ambaye alimwita Salama ili aweze kumsomea barua kutoka kwa
mwanawe Monika. Pia, vyuo na shule zilisaidiana na wazazi katika jukumu
la kuwalea na kuwakuza watoto wao. Mathalan, Bushiri aliandikiwa barua
ya kumwalika chuoni ili kwenda kujadiliana na mwalimu kuhusu maendeleo
ya mwanawe Ali shuleni.
Vijana wengine
kama vile walipoteza wakati wao katika shughuli za chama chuoni kuhusu
siasa badala ya kutilia maanani masomo bila kujali wala kubali kuwa
walikuwa wanasoma kwa msaada wa serikalina hata mwishowe Ali akaamua
kutumia madawa ya kulevya ili kuondoa usingizi agharamia wakati aliokuwa
ameupoteza kwani mtihani ulikuwa karibu kufanywa. Jambo hili lilikuwa ni
kinyume na kanuni za shule na mwishowe akalazimika kufukuzwa kutoka
shuleni.
Wanawake pia
walipewa nafasi sawa na wanaume katika uga wa masomo na kupata kazi ya
ajira kwani tunawaona Monika na Muna wakienda kusomea ng'ambo sawa na
Hasani na baadaye Monika anaajiriwa. Mighairi ya hayo, mhusika Karim
alikuwa anasomea Marekani lakini yeye hakuwa ameathirika na kukengeuka
kama Monika na maisha ya huko. Aliuhifadhi utamaduni wa jamii yake bila
kufanywa mtumwa na 'ustaarabu na maendeleo' ya huko.
Fauka ya hayo,
wafanyikazi waliweza kuisomea kazi waliyoifanya wakiwa kazini, k.m. Ali
na Rashid ili waweze kujiongezea ujuzi lakini kuna wale ambao hawakutaka
kusoma chochote baada ya kuhitimu na kupata kazi k.v. Hasani aliyechukia
kusoma zaidi. Kulingana na mifumo anuwai ya elimu, kuna mitihani ya
viwango mbalimbali shuleni, vyuoni na kazini ili kuzidisha ujuzi wao
kazini
Watoto waliweza kufunzwa heshima na tabia nzuri na
wazazi wakisaidiana na jamii.Hakuna mtu aliyemwacha mtoto wa mwenzake au
jirani kuelekea kubaya kwani mtoto alikuwa ni wa jamii nzima. Wawa wa
kike walifunzwa maisha ya ndoa na wazazi wa kike ilhali wavulana
walifundishwa kuhusu maisha ya ndoa na jinsi ya kuishi na wake na watoto
wao na wazazi wa kiume. .....Jopo
la Kiswahili, Starehe
|