|
Ukweli ni kuyasema mambo wazi kama yalivyo bila kuongezea wala
kupunguza lolote wala chochote. Kwa mara nyingi sisi waja hupendelea
kunena yasiyo ya kweli ili kujinufaisha wenyewe au mashoga wetu. Ni
kweli ni vizuri na bora hasa kuwa na utulivu wa moyo. Lakini je, ni
kwa nini tukae dhambini ili amani idumu?
Takribani aila yote ya wanadamu hujikuta katika hali ya ulaghai
aghalabu kila siku. Kwa wengi wetu, kunena uongo, kumekuwa kama
desturi. Ndio, jambo la lazima kama ibada kwao kutekeleza. Uongo
kwao ndio kiamsha kinywa, kishuka hali kadhalika chajio. Sisemi hata
usingizini huota urongo mtupu. Hawana matumaini kamwe ya kuutupilia
mbali upuzi huu na kuishi katika maisha ya ukweli na haki.
Limekuwa ni jambo muhali sana kwao kutamatisha kusema ukweli.
Ni jambo la kuhuzunisha tena la kusikitisha mno ikiwa sisi
walimwengu tulioumbwa na Rabana kwa mfano wake tena mikono yake
binafsi hatuwezi kuishi bila kuficha ukweli wa mambo. Je, kwani
aliyetuumba hakuwa na mipango kwa ajili yetu? Ni nani aliyesema na
tena ni wapi pameandikwa kuwa lazima tuuepuke ule ukweli ili kufaulu
aushini. Fahamuni dhahiri shahiri kuwa dhambi huzaa dhambi. Hakuna
mti mbaya huzaao matunda mazuri ya kutamanika. Haupo. La hasha!
Hivyo basi, kwa nini tunajidanganya wenyewe kuwa kwa kutosema ukweli
tutaweza twajiondolea masaibu?
Aghalabu wengi hawataniunga mkono. Nami aidha niko tayari kupingwa
lakini lazima na sharti ukweli usemwe. Ikiwa umewahi kuokoka kutoka
kwa masaibu fulani kwa sababu ya kudanganya, basi elewa kuwa hiyo si
bahati wala baraka. Usidhani kuwa hiyo ni njia ya kujiondolea
masaibu. Usifikiri njia ya uongo itakupeleka popote. Ni bora
kufahamu wazi wazi kuwa hilo si suluhisho kamwe. Na matunda yake ni
mabaya hata zaidi ya masaibu uliyoyaepuka, Na kwa kuwa shetani
ametufunga macho tusione mbele wala nuru yoyote, kwa sasa labda
hatuoni ubaya wake. Pengine hatuwezi kutambua madhara yake lakini
kama majuto, baadaye huja kinyume. Na njia za malipo ni tofauti.
Kumbuka jinsi ulivyojindoa mashakani kwa kuuficha ukweli!
Mwanzo
wa jarida Mwanzo
wa Kurasa za Kiswahili |