|
Hiyo
nomino kwa yakini inawavaa vilivyo. Nami ndivyo nilivyoamua kuwataja.
Mti huchongewa tundaze na matendo yao yanayowavika hili, nina
uhakika halitawapwaya na hatimaye kuwabwaga pu! Sakafuni kwa
kishindo. Na hata kijana anaweza
kumjua baba kabisa kabisa lakini asijue baba ni nini. Hayo ni baadhi
tu ya maswala tata ambayo hujitokeza hapa na pale katika kona za
njia hii ya safari ndefu ya maisha. Ni mara si moja ambapo watu huja
hadharani bila kutufahamisha kuwa dunia hii yetu yenye vyema na
vimbi inatia tamati. Hao ndio ninaowaita manabii wa uongo. Kama wewe
hukubaliani nami basi ukaniambie aliye mpachika mbwa jina hilo
angemwita kondoo?
Hawa jamaa wanaposema hivyo hawana
habari ya madhara abayo huyasababisha. Sisemi kuwa ni wanakanisa
ambao huishi pangoni tu bali wanasayansi wetu watukufu wameshawahi
naswa na mtego huu. Sio zamani sana walipotuarifu kuwa kuna jiwe
kubwa ambalo limekaa tahayatu kuja kwa udi na ambari kuigonga dunia
iwe vigae tupu. Hawakutuambia baadaye lilipoenda jiwe hili la ajabu
na ni nani aliye husika katika kulisukuma kando ili tunusurike. Kama
hawajaomba wanadamu msamaha basi nawajulisha wafanye hima kwani hata
mwana mpotevu alisamehewa.
Mimi nina haki na ilipotangazwa kuwa
dunia ingeisha mambo ya ajabu yalitokea. Hakuna binadamu ambaye
haogopi kifo na kila mmoja alipata kupiga bongo ili siku ya kiama
ijapo awe amelifanya hili na lile. Waliokuwa pengine taabani zaidi
ni wasomi. Shahada zao zote ambazo walikuwa wamezipigania na
kujitolea uhai na damu yao zingekuwa sawa sawia na matawi
yanayoanguka kutoka mtini, heri na makaratasi ya msalani! Wanakidato
cha nne na alama zao za kiwango cha ‘A’ hata nao muda wangelilia kwa
kuupoteza bure birashi. Waegezaji walisimama tisti wasijue la
kufanya kwa kuhofia kupoteza mali yao. Wakulima pia hawakuwachwa
nyuma kwa kususia shughuli zao kwani faida ingekuwa kwa ndege kama
wangeepuka mauti ya kiama. Kapera nao ndio waliharakisha kujipatia
jiko ili watimize hili na lile kabla ya kuiaga dunia kwa pamoja.
Kuna wengine walio na uwele wa kuogofya wa ukimwi na chanzo chake si
kingine bali ni nilichokueleza. Ni nani aliye shujaa kiasi kwamba
asilengwelengwe na machozi kisungura anapoyasikia haya? Binadamu
razini ni lazima machozi yamwende njia mbilimbili kapakapa. Na ni
nani anayesababisha haya kama sio hawa wanakundi ambalo jina lake
nalibana kwa sababu za kiusalama?
Sikatai kuwa dunia siku moja itaisha
katika andiko takatifu tunaarifiwa kuwa hata malaika wa mungu
hawataijua. Ninalohimiza ni kuwa chapa kazi wacha hofu. Vizazi na
vizazi vyaja na vitaondoka kabla ya kiama. Usije ukafa chanda ki
kinywani. Na kwa marafiki zangu, hata nyinyi tafuteni la muhimu
kuliko kueneza uvumi usio na msingi. Huu ni wosia ambao nimejitolea
mhanga kuwapasha la sivyo dunia yenu ikamilike kabla ya yetu na
mkitia nta masikioni, basi kumbuka mkataa la mkubwa husafiria
mtumbwi wa mfinyanzi. Inshala na Jalia awajaalie.
Mwanzo
wa jarida Mwanzo
wa Kurasa za Kiswahili |