|
Saa
moja imekwisha tangu Atinani kusimama kando ya mlango ule wa nyumba
ya baba Katosha. Sitahamala zinamwisha na machozi yanaanza
kumtiririka huku akimeza mafunda machungu ya mate. Kisha! Harufu!
Naam, harufu nzuri ya mkaango yenye mnato wa kuvutia inapitia
mapuani yake kutoka jikoni kwa Mama Katosha.
Kama afikiriavyo, chakula kitamu kama hiki alikila mara ya mwisho
miaka tisa iliyopita kabla ya mamake kuuliwa kinyama kando ya kanisa
alilokuwa akitumikia miaka nenda miaka rudi? Mbona? Alikataa
katakata kumuuzia tajiri mmoja bustani la kanisa lililotumiwa na
waumini kuombea sala maalum. Baada ya kifo chake, kitinda mimba wake
kaachiwa jukumu la kuiangalia familia. Kazi zilipomshinda kaka huyu,
yasemekana karukwa na akili na sasa huonekana akizururazurura
mitaani katika vichochoro vichafu huko jijini Nairobi.
Mkururo huu wa mawazo
unakatika pale aonapo Binti Katosha au Katosha mwenyewe. Hapa
Atinani anatumainia kupata suluhu. Alikuwa ametumwa na mamake wa
kambo kuomba chumvi. Si aombaye hupewa? Sasa alifahamu fika kuwa
asipopata chumvi chakula hakiliki. Sio kwa sababu kilikosa chumvi
bali alikosa chumvi! Mama kambo angemfoka kwa ghadhabu kisha
kumnyima chakula, ngo! Waama, hii ilikuwa siku yake ya tano tangu
atie chochote tumboni. Kama desturi aliagizwa na Mama Katosha
asimame pale kidogo huku akimtayarishia. Katosha amebeba
Jarida la Mwangaza akilisoma shairi liitwalo Likifungwa Lango,
shairi analopenda kulisoma sana kwa sababu anahofia huenda asiwe
ndani lango likifungwa na muumba. Potelea mbali! Watu wote
hawatatoshea Mbinguni!
Katosha amwulizapo
Atinani anataka nini, kabla ya kujibiwa " Chumvi", sauti yenye uzito,
ukali na ujeuri inasikika kutoka jikoni. "Mwaambie atoke! Hatuna
chumvi." Kwa unyonge na udhaifu, Atinani anaduwaa. Akatamani aondoke,
mguu ukakataa; aseme, mdomo ukakataa. Hapo alitazama lakini hakuona,
akasikiza bali hakusikia. Giza mchana! Dau la mnyonge haliendi joshi.
Hatimaye anazinduka na kurejea makwao. Alijua majukumu chungu nzima
yaliyomzunguka. Aoshe watoto na nguo zao, alishe mifugo, apalilie
shamba, atumwe kwa babuye kumpatia pesa zilizozotolewa Jumamosi
iliyopita wakati wa matanga ya dadake—Msichana wa darasa la tatu
aliyenajisiwa na kuuliwa kinyama na dume lisilotambulikana. Akh!
Dadake mkubwa naye ndiye huyo katalikiwa na mumewe! Kwa nini? Ana
dalili za kulisheheni gonjwa hatari la Ukimwi. Na mumewe je?... Sasa
dada huyu anaishi kwa mamake wa kambo anayemtesa sawa na Atinani
ambaye hamtambui kama mmoja wao na mara alisikialo jina la Atinani
huuliza "Ati nani?" Ama kweli dudu liumalo usilipe kidole.
Atinani afikapo
nyumbani anaambiwa ati hakuna chakula. Kisa? Akatumwa chumvi na
kuchukua siku nzima kurejea. Wakati huo anaanza kukumbushwa
majukumu yake ya siku ile. Mamamtu hapa anatoa orodha ya kazi hizi
kana kwamba anakariri shairi la beti saba. Isitoshe anamwongezea
jukumu jingine—kupunguza maji yaliyokuwa yameingia na kujaa shimoni
la choo. Shimo hili la futi nane lilichimbishwa Atinani mwenyewe.
Hii ilikuwa baada ya agizo la lazima kutoka kwa chifu wafanye hivyo,
baada ya babake Atinani kuuawa na ugonjwa wa Kipindupindu.
Ni wakati huu
anaposikia mlio wa mtoto mdogo kichakani kilichoitwa Bustani la
Kuzimu kwa kuwa kilijaa masaibu yasiyomithilika. Anamtambua mtoto
huyu—mwana wa dadake. Anamkimbilia huku akijiuliza maswali mengi. "
Kaenda vipi? Kaenda na nani? Na mamake yu wapi? Akimchukua mtoto
anaona amekumbatia kikaratasi. Anakichukua na kuinuka kukisoma.
Punde! Anaona vioja! Anatumbua mwisho wa dunia umefika. Dadake
kaning’inia mtini! Mauti! Kiza kikamzunguka Atinani. Mbele
hakuendeki wala nyuma hakurudiki. Kakitupa kile kibarua kando ya
mtoto na kukimbia akielekea upande wa kushoto. Macho yalikuwa
hayaoni. Lo! Yafungukapo anashtuka akitumbukia tumbwi! katika lile
shimo la choo lililojaa maji pomoni!
Hapo ndipo Atinani alitia kikomo cha
ghafula kutamatisha sentensi ya neno moja, Maisha. Maisha
yake yaliyojaa uchungu wa shubiri yalikuwa yamekamilika. Si kwake tu
bali yeye na aila yake yote isipokuwa mahasidi wake waliopania
kumtendea madhila aushini mwake. Katika Bustani la Kuzimu, wimbi
likawa limepita.
Mwanzo
wa jarida Mwanzo
wa Kurasa za Kiswahili |