|
Sekunde ya mwisho
ikawadia. Kengele na vipengele vya vigelegele na kelele tele
vikatawala kote. Tamasha zikawaka. Sasambua na aina zote za sherehe
zikatawala. Naam kasheheni vivinjo, shangwe, nderemo na furaha za
mpito mpito. Bila shaka ukawa ni mwaka mpya. Mwaka waliousubiria
wengi kwa hamu na ghamu. Mwaka wa 2007. Siku hii sherehe zikapita
kipimo! Wapenzi wakacheza wawili wawili huku wengine wakiamua
kusherehekea pekee kivyao. Ikambidi asiye na mwana aeleke jiwe.
Aliye na wivu na ajinyonge. Akishindwa ameze wembe bora asherehekee
mwaka mpya! Nao ukakaribishwa kote kwa hamukani za furaha.
Wengi wakaamua
kujiburudishia majumbani mwao. Nyumbani ni nyumbani! Wengine, "Ha!
Nyumbani hakuna hakunani." Nao wakaamua kwenda mijini. Safari za
hapa na pale. Haikosi kasababisha mauti si haba. Lo! Hao kakosa
mwaka mpya! Hawakujaliwa kuona angalau sekunde moja mwakani huu.
Rabuka awarehemu!
Basi ukawadia mwaka.
Naam, mwaka ambao kwa wengi, ungekuwa mwaka mkuu. Wakatarajia mengi
kuhusu huu mwaka. Sisemi wakadhani utakuwa na nguvu kiwango cha
uingiapo vipofu wakauona, usemapo viziwi wakasikiliza, uulizapo
mabubu wakajibu na uondokapo viwete wakauzindikiza. Ama kwako
ulikuwaje? Ukafika na ukawa mwaka wa saba tangu wakereketwa
waliokuwa na imani sisemi za kishenzi kujiingiza katika aushi ya
ufukara. Kwa nini? Ati kauza na kufuja mali yao wakiamini ati dunia
ingeisha mwaka wa 2000. Ole wao! Kwa Wakenya huu ulikuwa mwaka wa
arobaini na nne tangu kupata uhuru kutoka kwa mabeberu waliowakalia
na kuwafunika mzima mzima kama kifaranga yaini ambalo bado
kuanguliwa. Potelea mbali! Itatubidi tuyasahau yaliyopita na
kuyasozea kaburini kwani mavi ya kale hayanuki. Na Wakenya hao hao
ndio hao wanajilundika uwanjani ama ugani wa siasa mwakani! Sawa tu
bora wasifanye siasa za uchafu kama mazoea yao. Maskini akipata...
Mwaka huu ukawadia kwa
vituko, kasheshe na vitimbi. Kwa wengine ukawa kitantwariki—kichwa
chini miguu juu. Lo! Ukawatenganisha wapatanao, ukawapendanisha
wachukianao. Ukawashusha wajipandishao na wenye matao. Ukawaamsha na
kuwachomea blanketi waliokuwa wamelala. Ukawanyang’anya walioshika.
Ukawapatia waombao. Ukawapunguza wengi.
Kila masika huwa na mbu
wake. Gonjwa jipya la ajabu lenye dalili za kishetani likazuka. Hili
nalo ni Homa ya Rift Valley ukipenda, Bonde La Ufa Husambazwa
kupitia ulaji wa nyama za mifugo walioambukizwa. Ni gonjwa la
kuambukizanwa ambalo sijui katoka wapi. Lilianza tu kidogo kidogo na
sasa maovu yake yamekita mizizi kwani hata halina talasimu wala
hirizi. Tausia! Kuyakoleza madhila haya zaidi, adinasi wakayatenda
ya kuzighamidhisha keto za moyo. Saddam Hussein ndiye huyoo naye
tukamtia kitanzi. Akh! Tuyaache hayo ya maradhi kwani
yatatusereresha zaidi.
Licha ya mwaka hoi hoi
na shangwe zake, baadhi ya Wakenya wamebaki tu Wakenya. Hawabee
hawatee. Wangali katika hali ya ufukara na umaskini huku nao Ukimwi
ukiendelea kuwafagilia waliosalia. Nao uzembe haujawawauka. Kama
wasemavyo wengi, basi na tujikarambushe ili kuepuka kabisa masaibu
haya la sivyo yatatuangamiza kabisa! Nafsi zetu huenda zikabaki
dungudungu na asaa tukayadunisha maisha yetu ya halafu!
Mwaka wa elfu mbili na sita kwisha!
Buriani. Tugange yajayo sasa. Sisemi chochote. Ni bure bakhtata!
Hata hivyo waliozoea kusemasema hawasahau kusema kuwa siku njema
huonekana asubuhi. Basi kama ni ukweli wasemavyo hawa, basi
twautarajia mwaka huu kuwa mufidi zaidi tukiuliganisha na mingine
iliyotangulia.
Mwanzo
wa jarida Mwanzo
wa Kurasa za Kiswahili |