Mwangaza- Toleo la 14  
 
Maswali
Mabingwa
Jarida
Tuzo Letu
Mawaidha
Methali
Kamusi

Kukuru Kakara za Mwaka
Manabii wa Uwongo
Ukweli
Bustani la Kuzimu
Nasaha
Jina Bora
Uchambuzi wa Ushairi
Dosari Duniani
Mwaka Wetu mpya 2007
Muundo mpya wa www.gskool.com
Mashairi Yetu

Dosari Duniani na Chrispus Munywoki
 

Kwa yakini ni bayana kuwa dunia imebadilika na kuwa gunia. Watu wamekuwa viatu na wengine chatu. Sisemi utu umewatoka na badala yake kutu. Watoto wamekuwa watukutu nao watakatifu wasio watakatifu wakawa watakakitu.

Bila shaka utakubaliana nami kuwa nyakati hizi katika janibu nyingi, yameisha yamegeuka kabisa na hali yake imekuwa kigeugeu mithiliye kinyonga. Jambo hili linaathiri hususan wanadamu wala si wanyama. Ndio, waja waliopewa akili razini na maarifa kuliko kiumbe mwengine yeyote yule. Insi wameingiwa sijui na pepo gani. Uhayawani umetoka kwa wanyama na kustakimu miongoni mwa wanadamu. Ashakum si matusi.

Inadhihirika shahiri kuwa matendo tunayotenda hayana utu wowote. Na bado tuna akili timamu. Sikosi kustaajabu hata kama ya Firauni yako njiani yaja. Ikiwa akili zetu ni razini bila hitilafu yoyote ile, basi kwa nini aghalabu tunakata kauli kufanya jambo ambalo madhara yake twayafahamu fika. Ama yupo pepo ambaye huchangia katika uteuzi wetu? Kama yupo basi na ashindwe! Hata hivyo, pawe na athari ya mapepo au la hiyo sio sababu ya kufanya mambo maovu.

Maovu yamesheheni ulimwenguni. Mathalani mashoga wamekuwa mahasidi wakuu. Ni kwa nini mara nyingi unakuta kuwa, anayetarajiwa kuwa rafiki mkuu zaidi wa mtu huwa ndiye adui mkuu zaidi? Tazameni, mtu ana masahibu wake wanaomfaa kwa dhiki na faraja lakini huenda ikaja siku mwandani wake akamgeuka kinyama. Ni mara ngapi tumesikia shoga wa mtu akimgeuka na kuwa msaliti wake na kumfanya hata auliwe? Aidha imeshuhudiwa kuwa miongoni mwa wevi wanaovamia mtu aghalabu miongoni mwao huwa mtu anayefahamu vizuri na ndiye awaongozaye kutekeleza kitendo cha unyama kama hiki.

Tafakarini kukuru kakara za maisha katika ndoa. Ukimwuliza mke, atakwambia kuwa mtu anayemchukia zaidi ulimwenguni ni mumewe. Na hao ndio tunaowatarajia wapendane zaidi. Lakini kila usiku, sharti watapigana na kusemezana kwa maneno makali. Kila mmoja wao huishi kwa hofu amwonapo mwenzake. Kila mmoja anamsaka mwenzake. Madhumuni yao, wapambane. Maneno ya vitisho hufurika furi midomoni mwao. Waliokuwa chanda na pete sasa ndio hao wamekuwa mafuta na maji. Hawashirikiani tena. Maneno ya mapenzi yamekuwa ya matusi. Lo, upendo umekuwa uhasama jamani?

Bado tukiwa katika ndoa zenye doa, wazazi na wana hawasikilizani tena. Mwana aonapo baba moyo humwenda mbio na kumdunda ndu ndu ndu akihofia kupigwa. Yeye humwona mzazi kama jitu lililoumbwa kumletea dosari katika maisha yake. Wa aidha kunao ndugu katika jamii ambao hawasikizani tena.

Mwanzo wa jarida  Mwanzo wa Kurasa za Kiswahili

 


Haki zote zimehifadhiwa. Kunakili Makala yoyote kutoka Kwenye Tovuti Hii Bila Idhini Iliyoandikwa na Wakurugenzi Hakuruhusiwi. Makala yote yanamilikiwa na Gskool.com punde tu yanapotumwa.
Tuma Mchango wako
au maswali kwa kiswahili@gskool.com.
Home 
Forums and Discussions  Legal  Contacts  Faqs

©Gskool Educational Site